Askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kituo cha Mbagala, Koplo Riziki Mohamedi ambaye alikuwa amelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi) alifariki dunia jana saa 4 asubuhi alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Askari huyo aligongwa juzi asubuhi eneo la Mbagala Rangitatu akiwa anaongoza magari, ghafla gari aina ya Toyota Hiace inayofanya safari zake kati ya Temeke na Kongowe, lilishindwa kushika breki na kumgonga.
Ofisa Uhusiano Msaidizi wa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya fahamu, Moi, Patric Mvungi alithibitisha kufariki kwa askari huyo. “Huyu askari alilazwa Moi tangu jana (juzi) na amefariki leo (jana) saa 4 asubuhi,” alisema Mvungi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kienya Kienya, alisema utaratibu wa mazishi unafanywa.“Tuko kwenye majonzi na tunafanya maandalizi ya maziko, kwa sasa tunawasiliana na ndugu wa marehemu ili kujua atazikwa wapi na siku gani hivyo utaratibu ukikamilika tutawajulisha,” alisema Kienya.
Kienya alisema dereva wa gari lililomgonga askari huyo, liliyagonga magari mengine manne yaliyokuwa mbele yake na kusababisha watu sita kujeruhiwa.“Majeruhi hao walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani. Aliyeumia zaidi ni huyu askari,” alisema Kienya.
Alisema Polisi wanaendelea kumsaka dereva huyo ili aweze kufikishwa katika vyombo vya sheria, kwani alikimbia baada ya ajali kutokea